Hakiki riwaya ya Rosa Mistika (Euphase Kezilahabi)
kwa kutumia nadharia ya U-Marx.
Katika
utangulizi tutaanza kuelezea maana ya nadharia kutokana na wataalam mbalimbali
walivyoielezea, tutaangalia maana ya U-marx kutokana na wataalam mbalimbali. Na
tutajikita katika kuelezea misingi ya uhakiki wa ki-marx, kwa kutumia misingi hiyo tutahakiki riwaya ya Rosa Misitika na mwisho tutamalizia
na hitimisho.
Nadharia ni dhana
iliyofafanuliwa na wataalam mbailimbali kama ifuatavyo:-
Wafula na Njogu(2007) wanaeleza
kuwa nadharia ni “jumla ya maelekezo yanayomsaidia msomaji au mhakiki kuifahamu
kazi ya fasihi kwa kufuata utaratibu maalumu.” TUKI (2004) wanasema nadharia ni “mawazo, maelezo au muongozo ili
kusaidia kueleza,kutatua na kutekeleza jambo fulani.” Hii ina maana kuwa
msomaji kupitia nadharia anapata uwezo wa kufahamu mambo mengi kwa undani
ambayo anaweza kuyatumia katika kazi yake ya kifasihi.
Hivyo basi nadharia ni
taalumu inayojishughulisha na uchambuzi na uchanganuzi juu ya asili au mwazo wa
kitu au jambo fulani.
Dhana ya U-marx imeelezwa
na wataalamu mbalimbali kama ifuatavyo;Wamitila(2006) anasema U-marx ni falsafa
ya kiyakinifu hasa kwakuwa pana msisitizo mkubwa kwenye msingi wa hali za
kiyakinifu za maisha kama mazingila ya kuishi kuliko mawazo katika maisha ya
binadamu. Ikimaanisha kwamba mawazo yake hayategemezi kwenye dhana dhahania
kama urembo,ukweli au ndoto bali anayategemeza kwenye uhalisia unaonekana. Nadharia
ya U-marx ilianzishwa na Karl Marx mwaka 1818-1863 na Fredrick Engles mwaka
1820-1895.
Katika kutekeleza nadharia ya U-marx kuna misingi ya kufuata ili kuhakiki kazi za kifasihi kwa
ufasaha. Moja, misingi hiyo ni historia ya maisha ya binadamu inayoweza
kuelekeza katika misingi yakinifu ya kiuchumi; ambayo itachunguza njia ya
uzalishaji mali pamoja na miundo ya kiuchumi inayo athiri uzalishaji mali na
usambazaji wa mali hizo. Pili, kuamini kuwa historia ya kibinadamu
inadhihirisha au kuakisi harakati zinazo endelea katika matabaka ya
kiuchumi-jamii; matabaka hayo yapo katika ngazi ya familia, dini na elimu na
tatu, ubepari kama njia ya uzalishaji mali na mara nyingi huharibiwa na tabaka
la chini.
Kulingana na misingi ya ki-marx ,
tunaweza kuhakiki Riwaya ya Rosa Misitika iliyoandikwa na Euphrase Kezilahabi kama ifuatavyo:-
Suala la dhuluma na unyanyasaji; unyanyasaji
ni kitendo cha mtu mwenye nguvu au shirika fulani kuwakandamiza watu wasio na nguvu
katika familia au jamii fulani inayowazunguka
na dhuluma ni kitendo cha mtu au watu kunyimwa haki zao za msingi. Kupitia
msingi wa nadharia ya ki-marx inaonesha suala la ubepari kwamba ni jumuisho
katika suala la dhuluma na unyanyasaji. Mwandishi anawatumia wahusika Flora,
Stella, Honorata, Sperantia na Emmanuel walivyodhulumiwa kwa kunyang’anywa vitu vyao vyote baada ya wazazi wao kufariki. Katika
uk.96, msanii anasema:-
“Hawa jamaa walirithi. Walirithi hawa jamaa.
Walirithi, walirithi. Jamaa waligawana vitu. Walirithi kila kitu kilichokuwa
ndani ya nyumba. Walirithi michungwa na miembe. Walirithi migomba yote.
Walirithi paka na mbwa. Walirithi majani yaliyokuwa juu ya paa, na miti yote,
iliyofanya nyumba isimame. Walirithi mashamba yote. Walirithi kuku, kweli
walirithi. Lakini hapakuwa na mtu hata
mmoja aliyeweza kusema atamchukua mtoto fulani amtunze.”
Vilevile msanii anaonesha
suala la unyanyasaji kwa kumtumia mhusika Regina anavyonyanyaswa na
mumewe. Mfano katika riwaya ya Rosa Mistika suala la unyanyasaji limejitokeza
katika sehemu ya kwanza uk. 3 mwandishi anaposema:
‘‘Lakini
Regina tangu aolewe hakuwa na raha ;alikuwa akisumbuliwa na kuteswa na mumewe
kwa kosa lisilo lake.”
Wanawake
wengi katika jamii zetu wamekuwa wakinyanyaswa na waume zao kwa
kupigwa na kupewa majukumu yote ya familia bila ya kusaidiwa na waume zao.
Nadharia ya u-marx
inazungumzia suala la unyanyasaji na dhuluma kuwa ni tatizo kubwa katika jamii
hasa katika kufanya maendeleo ya kijamii ili jamii iweze kujikomboa kiutamaduni ,kisiasa na kiuchumi.
Vilevile suala la uongozi mbaya, uongozi mbaya ni
kitendo cha viongozi kushindwa kukidhi mahitaji ya watu wake. Pia suala hili la
uongozi mbaya ni moja kati ya suala zima la ubepari ambalo huleta mikururo
katika jamii, hivyo mwandishi anaonesha uongozi mbaya kwa kumtumia mhusika
Deogratias pale anapo kuwa anatumia cheo chake vibaya kwakuwa kandamiza watu. Uk.
41 mwandishi anasema:-
“Zaidi
ya hayo,Deogratias alikuwa mmoja kati ya wale watu watumiao vyeo vyao na pesa
kwa kutaka chochote wapendacho.”
“...Nasikia
alikwisha wapa mimba watoto wawili wa shule? Ndiyo, lakini aliwapa shilingi
wasimseme. Walitaja vijana wengine waliokuwa wakisoma nao.”
Pia
suala la uongozi mbaya lipo hata katika jamii zetu kwani kuna baadhi ya
viongozi ambao hutumia nafasi zao kufanya vitu visivyostahili katika jamii
mfano rushwa ya ngono, matumizi mabaya ya fedha za serikali.
Katika nadharia ya
U-marx inasema kwamba ili jamii iondokane na uongozi mbaya ni lazima jamii ipambane kuondoa uongozi mbaya.
Pamoja na hayo suala la migogoro mwandishi amelionesha; migogoro
ni mvutano au ukinzani baina ya mtu na mtu au pande mbili. Migogoro imegawanyika
katika makundi mbalimbali mfano migogoro ya kinafsi, mtu na mtu, mtu na
serikali au jamii yake. Katika riwaya hii mwandishi anaonesha jinsi jamii ya
watu wa Ukerewe wanavyokumbwa na mikururo katika jamii hiyo. Mwandishi
anamtumia mhusika Rosa anavyokua na mgogoro na baba yake kutokana na
malezi aliyokuwa anapewa na baba yake. Katika uk. 58 mwandishi anasema:-
‘’Zakaria
alipata maneno yote: maneno aliyopaswa kuambiwa siku ile……Rosa tangu leo wewe
si mototo wangu. Tangu leo wewe si baba yangu. Rosa alidakia bila kukawia.
Aliingia mara moja ndani ya motakaa na kwenda zake Beach. Siku hiyo Rosa
hakurudi nyumbani.”
Suluhisho la mgogoro
huu ni Rosa kuondoka na kutokurudi nyumbani.
Mgogoro mwingine ni
kati ya Regina na Zakaria kutokana na
suala la ulevi wa Zakaia ambae ni
mume wa Regina. Uk. 4. Mwandishi anasema:-
‘’Mwanzoni
haya yalikuwa yakizunguka kichwani mwake aliposikia sauti kwa mbali: Hoi! Hoi!
Hoi! Alifahamu. Alifahamu huyo mtu alikuwa nani na alikuwa katika hali gani:
sauti hiyo alikwishaizoea.’’
Mgogoro huu haukupatiwa
suluhisho kwani Zakaria aliendelea na tabia yake ya ulevi mpaka mauti yalipomchukua.
Vilevile mwandishi
anaonesha mgogoro wa nafsi kwa kumtumia mhusika Rosa, baada ya kukataliwa
kuolewa na Charles. Mwandishi anasema;
“Ha!
Rosa, kweli wewe ulikuwa bikira! Unafikiri baada ya kufahamu kwamba ulichezewa
sana huko Morogoro,na baada yangu mimi mwenyewe kuona bonde la ufa na kuliona
hilo sikio,unafikiri mimi ninaweza kukuoa! Ha! Dada yangu,sahau.’’uk 90
Suluhisho la mgogoro
huu ni Rosa kuchukua maaamuzi ya kujiua.
Kwa mujibu wa ki-marx
migogoro haina budi kuwepo katika jamii na ni lazima pawepo migogoro ndani ya
jamii yeyote, hivyo ni lazima itafutiwe suluhisho ili kuleta maendeleo.
Vilevile suala la
matabaka; matabaka ni utofauti uliopo kati ya mtu na mtu au jamii na serikali.
Katika jamii kuna
matabaka ya aina mbili ambayo ni tabaka la juu na tabaka la chini katika mfumo
wa uzalishaji mali yaani kiuchumi,kisiasa na kiutamaduni. Mwandishi anaonesha
suala hili jinsi linavyojidhihirisha wazi kati ya wenye nacho na wasio nacho
mfano familia ya Zakaria hawa ndio wasionacho uk.38, mwandishi anasema:-
‘’…Walianza
kufikiri, akija atalala wapi? Mgeni-mkubwa na mwenye heshima namna hiyokulala
naye ndani ya nyumba moja isiyo na vyumba vingi lilikuwa jambo la aibu.”
Pamoja na hayo wapo wenyenavyo ni kama vile
Mkuu wa wilaya Deogratus uk.41,
“Nasikia
alikwisha wapa mimba watoto wawili wa shule? Ndiyo, lakini aliwapa shilingi
wasimseme. Walitaja vijana wengine waliokuwa wakisoma nao.”
Watawala mfano kiongozi Mkuu wa wilaya uk. 58
na watawaliwa ni Zakaria na Ndalo. Tatu,matabaka kati ya wasomi na
wasiosoma, wasomi kama Rosa,Stella na Charles, wasiosoma ni Regina uk. 46.
Suala hili la matabaka
katika jamii zetu bado linaendelea, hivyo kwa mtazamo wa kimarx unatoa
pendekezo kuwa ili jamii ijikomboe na matabaka lazima ifanye mapinduzi.
Vilevile suala la uzalishaji
mali, uzalishaji mali huo unaweza kuwa katika nyanja za kiuchumi,kisiasa,kiutamaduni
na kijamii .Mfumo wa uzalishaji mali kwaujumla huzingatia katika uletaji
maendeleo ya mtu binafsi au nchi kwa ujumla. Katika riwaya hii mwandishi anaonesha jinsi mhusika Zakaria navyoshindwa kufuatilia
vitu ambavyo vinaweza kumkomboa yeye pamoja na familia yake badala yake
anaendekeza ulevi ambayo siyo njia sahihi ya uzalishaji mali. Katika uk. 17,
mwandishi anasema :-
‘’Aaa!
Aaa! Pombe ilikuwa ya kutuua. Hivi tulikunywa chupa ngapi? Zakaria aliuliza.
Mimi nakumbuka tulikunywa chupa kumi.”
Kitendo hiki hata
katika jamii zetu bado kipo kwani watu wengi hujihusisha na masuala ya ulevi
kuliko kujihusisha na masuala ambayo ni tija katika uzalishaji mali.
Hivyo ili mhakiki wa
kazi za kifasihi aweze kufanya kazi yake
vizuri ni lazima atumie nadharia zaidi ya moja ili aweze kuhakiki vipengele vyote vya fani na maudhui, kwani
kipengele kimoja hakiwezi kujitosheleza katika kuhakiki kazi ya kifasihi.
MAREJELEO
Kezilahabi, E. (2011). Rosa Mistika. Nairobi:
Kenya Literature Bureau
TUKI. (2014). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Dar
es salaam: O.U.P East Africa Limited.
Wamitila, K. (2002). Uhakiki wa Fasihi, Misingi
na Vipengele vyake. Mombasa: Phoenix Publishers Limited.
maeleo mazuri na ambayo yanaeleweka kwa urahisi. Yamenfaa sana
ReplyDeleteKazi nzuri inafaa
ReplyDelete